Familia ya Wilson Kabwe, aliyekuwa mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, imesema ndugu yao alishawatoa wasiwasi kuhusu tuhuma zilizosababisha kusimamishwa kazi na Rais John Magufuli na kwamba alitamani uchunguzi ufanyike haraka ili ukweli ujulikane.
Kabwe
aliyefariki dunia Mei 20 kwa ugonjwa wa saratani ya tezi dume jijini
Dar es Salaam, alisimamishwa kazi na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa
daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni Aprili 19.
Miongoni
mwa makosa yaliyosababisha kusimamishwa kwake ni madai ya kusaini
mkataba kwa kutumia sheria ndogo ya mwaka 2004 kutoza magari yanayotoka
kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo (UBT) Sh4000 na mwingine wa Sh8,000
chini ya sheria ndogo mwaka 2009.
Kulikuwa
pia na madai ya kukithiri kwa rushwa katika kituo hicho hasa katika
kutoa magari na ukodishwaji wa vyumba vya kupangisha, kinyume na
utaratibu na kuongeza muda wa mzabuni aliyeingia mkataba na jiji wa
maegesho ya magari.
Akizungumza
jana nyumbani kwao, Masaki jijini Dar es Salaam, mtoto wa marehemu,
Joseph Kabwe alisema kifo cha baba yao hakikutokana na mshtuko wa
kusimamishwa kazi, bali alianza kuugua muda mrefu na alishawaambia kuwa
hana wasiwasi na tuhuma hizo, bali anataka uchunguzi ufanyike haraka.
“Alikuwa
na saratani ya tezi dume na alikuwa akitumia dawa za chemotherapy
ambazo ni kali sana na zilisababisha kuathirika kwa ini. Hata siku baba
anatumbuliwa pale darajani alisema hana wasiwasi kwa sababu kila kitu
kiko sawa sawa,” alisema Joseph.
“Baba
alitutaka tusiwe na wasiwasi, tena mwenyewe alikuwa akisisitiza kuwa
anatamani matokeo ya uchunguzi yatoke mapema ili ukweli ujulikane,” alisema.
Jana
msibani kulikuwa na viongozi tofauti wa ngazi ya mkoa waliofika kutoa
pole. Kaimu mkurugenzi wa jiji aliyekuwapo msibani hapo, Sarah Yohana
alisema Halmashauri ya Jiji inashiriki msiba huo kwa kuwa Kabwe alikuwa
mtumishi wao.
“Yule
alikuwa mtumishi wa halmahsauri na ana haki zake kama mtumishi mwingine
yoyote. Tutatoa jeneza, gari la kusafirishia maiti, chakula na
rambirambi,” alisema Sarah.
Sarah
alisema alikabidhiwa ofisi na Kabwe tangu Novemba mwaka jana baada ya
kwenda kutibiwa nchini India. Kuhusu taratibu za utumishi, alisema licha
ya Rais kumsimamisha kazi, hawakuwahi kuona barua yoyote iliyoletwa
inayohusu kusimamishwa kwake.
“Inawezekana
alipewa kwa njia nyingine, lakini sisi hatukuona barua ya kusimamishwa.
Yule ni ‘presidential appointee’ (mteule wa Rais), yeye ndiye mwenye
mamlaka na watu wake wa kufanya uchunguzi. Sisi hatujui, inawezekana
wanafanya uchunguzi wao huko wenyewe,” alisema Sarah.
Jana
Msemaji wa familia hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Eliab Mkenga
Kabwe alisema hawana ugomvi wowote na Serikali huku akimkana mtu
aliyejitambulisha kuwa msemaji wa familia hiyo, Dk. Zawadi Machuve
aliyetoa maelezo kwa waandishi wa habari juzi kuwa hawataki viongozi wa
Serikali wakanyage msibani.
Aliongeza kuwa familia hiyo inatambua na kuthamini mchango wa Serikali katika kugharamia matibabu na huduma zote za mazishi.
Alisema
Makonda aliyetoa tuhuma za Kabwe kabla ya Rais Magufuli kutangaza
kumsimamisha kazi, anatarajiwa kufika msibani hapo muda wowote.
“Mkuu
wa Mkoa, Makonda bado hajafika hapa, lakini anaweza kufika wakati
wowote. Unajua yeye ndiye mwenye mkoa wake kwa hiyo atafika tu wakati
wowote,” alisema.
Mbali
na viongozi wa jiji waliokuwapo kwenye msiba huo, viongozi wa mikoa
mingine akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo na mkuu wa wilaya
ya Nyamagana, Baraka Konisaga walikuwapo msibani hapo.
Mbunge
wa Ubungo, Saed Kubenea, ambaye alikuwapo eneo hilo, ameshauri msiba
huo uhamishiwe katika ukumbi wa Karimjee ikiwa ni kumpa heshima Kabwe
aliyekuwa kiongozi wa jiji, lakini hakuna dalili za kufanya hivyo.

No comments:
Post a Comment