Monday, May 30, 2016

Mke wa Trafiki Kinyogori Adaiwa Kukiri Kumuua Mumewe


MKE wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Ally Salum (Kinyogori) aliyeuawa hivi karibuni, inadaiwa amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo, akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke mwingine.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.

Wakati huo huo, Kamanda Sirro amezungumzia pia mauaji ya Anathe Msuya yaliyofanyika hivi karibuni Kigamboni na kusema polisi inaendelea kumtafuta msichana wa kazi za nyumbani aliyetoroka siku moja kabla ya kifo cha mwanamke huyo.

Anayetuhumiwa kuua mumewe 
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Dar es Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya awali mke wa Kinyogori amekiri kuhusika.

Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake kwa sababu za kipelelezi, aliamua kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke mwingine.

“Ni jambo la kusikitisha kuona mtu anatoa uhai wa mtu sababu ya kuachwa. Tunawasihi wananchi kuepuka kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu tu ya kuachwa wanawake wapo wengi na wanaume wapo wengi unaweza kuachwa na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai wa mtu,” alisisitiza Sirro.

Hata hivyo, Sirro alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili waweze kuwataja watu wengine walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya kuonekana kuwepo kwa wahusika wengine.

‘Hausigeli’ asakwa 
Kuhusu mauaji ya Anathe aliyechinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Kamanda Sirro alisema wanaendelea na jitihada za kumtafuta msichana huyo ahojiwe kuhusu tukio hilo.

Aidha alisema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo huku polisi ikiwa imeandaa timu ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo kufanikisha kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.

Sirro alisema msichana huyo aliondoka siku moja kabla ya tukio hilo la mauaji hivyo kupatikana kwake, kunaweza kusaidia polisi kujua kama kuondoka kwake kulikuwa salama au kuna kitu kimejificha.

“Msichana huyu tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka salama na kumhoji zaidi juu ya kuondoka kwake siku moja tu, tukio linatokea nina imani tutafanikiwa kumpata na wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema Sirro.

Mamia wajitokeza msibani 
Vilio na simanzi jana vilitawala wakati mamia ya wakazi wa Kibada Kigamboni na Salasala walipokuwa wakiuaga mwili wa marehemu Anathe Msuya (30), aliyeuawa Mei 25 nyumbani kwake kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.

Mwili ulichukuliwa jana asubuhi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa nyumbani kwake Kibada, kwa ajili ya kuagwa na majirani zake kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa mkoani Arusha leo.

Akizungumza baada ya mamia kumuaga nyumbani kwa marehemu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyakwale Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani waliomba familia wapate fursa ya kumuaga jirani yao ambaye tangu ahamie ana muda wa miezi sita.

“Baada ya kuambiwa msiba upo Salasala tuliomba kama majirani na sisi tupatiwe fursa ya kuuaga mwili wa ndugu yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa kweli msiba wake umetusikitisha sana” alisema.

Akizungumzia tukio hilo alisema kuwa mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4) aliwataarifu majirani kuwa mama yake haamki na ndipo walipofika wakakuta ameuawa.

Mwenyekiti huyo alitoa pole na kusema atahakikisha wanaimarisha ulinzi na kuhimiza wenye viwanja ambavyo havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama.

Thursday, May 26, 2016

Rais Magufuli Akemea Vitendo vya Rushwa kwa Wakandarasi Wazawa.. .....Awataka Watangulize Mbele Maslahi ya Taifa


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi kote nchini kufanya kazi kwa kutanguliza maslai ya taifa, badala ya kutaka kupata faida kubwa kupita kiasi kutoka kwenye zabuni za miradi ya ujenzi wanayopata kutoka serikalini.

Dkt. Magufuli amesema hayo leo tarehe 26 Mei, 2016 alipokuwa akifungua mkutano wa mashauriano wa bodi ya usajili wa wakandarasi kwa mwaka 2016 unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli amesema serikali yake ipo tayari kuwapa kipaumbele wakandarasi wa Tanzania pale inapotangaza zabuni za miradi ya ujenzi, lakini amewataka kujirekebisha kwa kupanga viwango vinavyostahili vya gharama za ujenzi wa miradi hiyo ambavyo serikali itaridhika.

“Nawatolea mfano, idara ya mahakama imetangaza kujenga mahakama za mwanzo na za wilaya, kwenye bajeti wana shilingi bilioni 24, makadirio ya kitaalamu yanaonesha kila jengo lisizidi shilingi milioni 200, wakandarasi wazalendo walipoomba katika nyaraka zao wametaka jengo moja lijengwwe kwa shilingi bilioni 1 na milioni 400, sasa nakuuliza Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu wakandarasi, hata kama una upendeleo, upendeleo huo utapasua moyo.

“Hata kama utakuwa na upendeleo kiasi gani kwa wazalendo utashindwa, sasa mimi niwaombe ndugu zangu wakandarasi, pamoja na nia nzuri ya serikali kuwasaidia wakandarasi wazalendo ni lazima na ninyi muwe na nia nzuri ya kuisadia nchi” Amesema Rais Magufuli

Pamoja na hilo, Rais Magufuli ametaka wakandarasi hao kuacha kutoa rushwa kwa watendaji wa serikali pale wanapoomba zabuni za ujenzi na badala yake amewataka kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) ili watendaji hao wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Mimi niwaombe wakandarasi, msikubali kutoa rushwa, na muwafichue watendaji wanaoomba rushwa, atakapokuomba wewe rushwa hujui amewaomba wangapi, na utakapotoa rushwa huna hakika kama ile tenda utaipata, wengine wameishia kutoa rushwa hapa, rushwa hapa, rushwa hapa mpaka anafilisika, kazi huipati na rushwa umeitoa” Amesisitiza Dkt. Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa wakandarasi hao kujipanga ipasavyo ili waweze kupata zabuni katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi itakayofanywa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga hapa Tanzania, Ujenzi wa Reli ya Kati na Ujenzi wa Viwanda.

“Sina uhakika kwamba mmejipangaje wakandarasi wa Tanzania katika kuhakikisha hiyo kazi mnaipata ya kujenga bomba kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.

“Nitasikitika sana kilometa zote 1,410 pasiwepo mkandarasi hata mmoja wa kutoka Tanzania, wenzetu wanajipanga, na ninavyoona wakandarasi wa Tanzania wameendelea sana, lakini nashindwa kuelewa kuna tatizo gani linatufanya kutojua changamoto zinazotukabili, tumejipanga kujenga reli ya kati (Standard Gauge) kwenye bajeti ya mwaka huu tunaanza na kilometa 100, lakini kuna fedha nyingine zitatolewa na serikali ya China, tutajenga zaidi ya kilometa 1,200 (Standard Gauge, Central Corridor) itakayounganisha Mwanza, Kigoma, Burundi na Rwanda. Wakandarasi wa Tanzania mmejipangaje? " ameuliza Rais Magufuli.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola ambaye amesema Taasisi hiyo ipo tayari kukabiliana na rushwa iliyopo katika sekta ya ujenzi ambayo ni miongoni mwa sekta zenye rushwa kubwa na ametaka wakandarasi watoe ushirikiano kukomesha tatizo hilo.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

26 Mei, 2016

Lowassa Ajisafisha Tuhuma za Kukwapua ardhi Ya Wananchi na Kujimilikisha


Siku chache  baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kulieleza Bunge kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alijimilikisha shamba la Makuyuni Wilayani Monduli mkoani Arusha, Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga amejitokeza kutoa ufafanuzi unaomsafisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Kalanga alisema kuwa Lowassa hamiliki shamba hilo la Makuyuni kwakuwa tangu Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alipofuta hati ya umiliki wa shamba hilo kutoka kwa raia wa Kigeni aliyemtaja kwa jina la Stein, bado halijamilikishwa rasmi kwa wananchi na ndio ilikuwa hoja yake.

Alisema kuwa maelezo ya Lukuvi hayakuwa na ukweli  na kwamba alichanganya kati ya shamba hilo la Mkuyuni na shamba la Manyara Ranchi ambalo hati yake ilifutwa tangu mwaka 2000 na kukagawiwa kwa wananchi wa Monduli ambapo Lowassa alisaini hati miliki yake kama muwakilishi wa wananchi wa Wilaya hiyo kwakuwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya udhamini ya Ardhi (Tanzania Land Trustee (TLCT).

“Jambo la kushangaza ni pale Waziri alipochanganya shamba hilo na lile la Manyara Ranchi ambalo hati yake ilifutwa tangu mwaka 2000 na kugawiwa kwa wananchi. Hati miliki ya shamba hilo la Manyara Ranchi ilisainiwa na Lowassa ambaye wakati huo alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Land Trustee(TLCT),” alisema

Awali, Waziri Lukuvi alieleza kuwa Shamba hilo la Mkuyuni linapaswa kumilikishwa kwa wananchi lakini nyaraka zinaonesha kuwa hati yake imesainiwa na Lowassa na kwamba Serikali itamnyang’anya na kulirejesha kwa wananchi.

Juzi, Lowassa aliahidi kuwasiliana na Mbunge huyo ili kufuatilia kauli aliyoitoa Waziri Lukuvi dhidi yake kuhusu kujimilikisha shamba hilo ili aweze kutoa ufafanuzi kwani hakuna ardhi anayoimiliki kinyume cha taratibu.

Wednesday, May 25, 2016

Jeshi la Polisi Zanzibar Lawatahadarisha Viongozi wa CUF

Jeshi la Polisi Zanzibar, limesema kuwa vitendo vya kihalifu vya uvunjifu wa amani vinavyotokea kisiwani Pemba vinachochewa na viongozi wakuu wa chama cha Wananchi CUF.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa, naibu mkurugenzi wa upelelezi na Makosa ya jinai wa Jeshi hilo, Salum Msangi alisema kuwa viongozi wakuu wa CUF wamekuwa wakiwatuma wafuasi wao kufanya vitendo vya hujuma kisiwani Pemba kwa madai kuwa serikali iliyopo madarakani sio halali.
 
Alisema kuwa jeshi la polisi linataarifa za uhakikia kuhusu viongozi wa CUF wakiwapongeza wafuasi wao na kuwapa zawadi ya fedha kwa kuweza kufanya vitendo vya hujuma kisiwani humo ikiwemo uchomaji moto wa majengo mbalimbali na kuhujumu mikarafuu na mazao mbalimbali.
 
“Tunao ushahidi viongozi wa CUF wamewakusanya wafuasi wao na wanawapa pongezi wale ambao wameza kufanikiwa kufanya vitendo vya hujuma dhidi ya wananchi”alisema.
 
Alisema kuwa jeshi hilo halitamvumilia mtu yoyote atakaehusika kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani na wala halitakua na muhali katika kuchukua hatua za kisheria bila ya kujali cheo cha mtu.
 
Aidha alisema kuwa jeshi hilo linawashikilia watu zaidi ya 20 kisiwani Pemba ambapo wanahusishwa na vitendo vya uvunjifu wa amani na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
 
Akizungumzia kuhusu ripoti ya Chama cha wananchi CUF waliyoitoa juzi ya kulipeleka Jeshi hilo mahakama ya kihalifu ya kimataifa (ICC),alisema jeshi hilo haliogopi kupelekwa huko na kusema kuwa taarifa zilizomo katika ripoti hiyo zinazohusu jeshi la polisi ni za uongo.
 
“Kama ICC tutaanza kuwapeleka wao viongozi wakuu wa CUF ambao wao ndio wachochezi wakubwa wa uvunjifu wa amani ya nchi na taarifa zao zote tunazo”alisema Msangi.
 
Hata hivyo alisema jeshi la polisi linaendelea kuwaita watu mbalimbali na kuwahoji akiwemo Katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho.
 
Jeshi hilo liliwapa tahadhari viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa kuacha tabia ya kuwashawishi wafuasi wao kufanya vitendo vya hujuma wakati wao wametulia majumbani mwao.

Bunge Latolea Ufafanuzi Madai ya Kitwanga Kujibu Swali Bungeni Huku Akiwa Amelewa


BUNGE limekanusha taarifa inayosambazwa katika mitandao ya kijamii na watu wanaodaiwa kuwa ni madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Taarifa hiyo inadai kuwa video iliyomuonesha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akijibu swali bungeni Mei 20 mwaka huu, ilihaririwa na kusambazwa na maafisa wa Bunge.

Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge kilitoa taarifa ya ufafanuzi kuhusu madai ya kuhaririwa kwa video hiyo, mjini Dodoma jana.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa taarifa hizo, si za kweli na zina lengo la kuupotosha umma, kwani ukweli ni kwamba kipindi cha maswali na majibu bungeni, hurushwa moja kwa moja na hupatikana kupitia vituo vyote vya televisheni, vinavyopokea matangazo ya bunge.

Ilisema matangazo hayo, yanaweza pia kurekodiwa na mtu yeyote mwenye uwezo huo popote alipo, kadri anavyoweza kuyapokea matangazo.

Advertisement

Tuesday, May 24, 2016

China yakana kuuza nyama ya binaadamu Afrika



160523165133_cornedbeef2Wizara ya maswala ya kigeni nchini China imekana ripoti kwamba kampuni za chakula nchini humo zinaweka nyama ya binaadamu na kuuza barani Afrika kama nyama ya ng’ombe.
Chombo cha habari nchini humo Xhinua kimesema kuwa jarida moja nchini Zambia lilimnukuu kimakosa mwanamke mmoja ambaye hakutajwa anayeishi China.
Alisema kuwa kampuni za China zilikuwa zikichukua miili ya wafu kuitia katika viungo na kuiweka katika mikebe.
Msemaji wa China Hong Lei amesema kuwa ripoti hizo hazina uwajibikaji.

Balozi wa China nchini Zambia,Yang Youming ,amesema kuwa ripoti hizo zililenga kuharibu uhusiano mzuri kati ya mataifa hayo mawili.
“Leo jarida moja linasambaza uvumi , likidai China inatumia nyama ya binaadamu ambayo uihifadhi katika mikebe na kuiuza Afrika.
”Hii ni dhulma ya makusudi ambayo haiwezi kukubalika kabisa kwetu sisi”

Maalim Seif Sharif Hamad Aitwa Polisi Kuhojiwa

Jeshi la Polisi Zanzibar litamhoji Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad Ijumaa ya wiki hii kuhusu masuala mbalimbali ambayo hata hivyo, hayakuwekwa wazi.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame alisema jana: “Natambua kuwa wasaidizi wangu watazungumza naye Ijumaa. Wao ndiyo wanajua watamhoji nini.”

Alipoulizwa kuhusu mahojiano hayo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi naye hakuweka wazi badala yake alisema kuna masuala mengi ambayo ofisi yake inahitaji kuyafahamu kutoka kwa Maalim Seif.

Hii ni mara ya kwanza kwa Maalim Seif kuhojiwa na polisi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ambao kwa Zanzibar ulirejewa Machi 20, baada ya ule wa Oktoba 25 mwaka jana kufutwa.

Maalim Seif ambaye kabla ya uchaguzi huo alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alipinga kurudiwa kwa uchaguzi huo msimamo ambao pia ulichukuliwa na chama chake.

Kiongozi huyo amekuwa akitoa matamko kadhaa ya kuwashawishi wananchi kupinga utawala wa Serikali iliyopo madarakani.

Akiwahutubia wafuasi wake huko Pemba hivi karibuni, Maalim Seif alisema Serikali ya CCM imeanza kutikisika kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na hatua ya chama chake CUF kutowatambua viongozi wake pamoja na Serikali. 
“CCM wajue wamekalia kuti kavu, siku yoyote wataanguka... tufanye kazi mpaka haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu hawana safari ya kudumu,” alisema.

Aliwataka wanachama wake kuonyesha kwa vitendo kutoitambua Serikali ikiwamo kukataa kulipishwa kodi za ovyovyo pamoja na kujitenga na viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mfano tunaweza kuamua siku fulani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo vyote vya usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima kuonyesha hatuitaki Serikali ya CCM,” alisema huku akishangiliwa na umati uliofurika katika ofisi za chama hicho.

Mapema jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kuwa amesikia juu ya wito huo lakini hakuwa amepata taarifa rasmi kutoka kwa mkuu wake.

“Nimesikia kama mlivyosikia ninyi,” alisema na kuongeza: “Nimeelezwa pia hata leo Kamishna wa Polisi Zanzibar alikuwa na mahojiano naye.”

Kuhusu hilo Kamishna Makame alisema: “Sijaonana wala kuzungumza naye leo. Hiyo si kweli.”

Juzi, wakati akizindua ripoti ya Uvunjifu wa Haki za Binadamu uliofanyika visiwani humo kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema wanazo taarifa za Serikali kutaka kuwakamata viongozi waandamizi wa chama hicho na kuwashikilia.
Alisema wamebaini mpango wa kukamatwa kwao na kuwekwa kwenye Mahakama za bara ili kuwanyamazisha Wazanzibari.

Monday, May 23, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya May 24

Rais Magufuli Afanya Uteuzi wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mshauri wa Rais Katika Masuala ya Uchumi

Watu zaidi ya 10 wahofiwa kufariki ziwa nyasa



Taarifa ya awali iliyoripotiwa na kituo cha television cha ITV muda mfupi uliopita imeeleza kuwa watu zaidi ya 10 wanahofiwa kufariki dunia katika ziwa nyasa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kutoonekana kwa siku mbili huko Mbamba Bay mkoani Ruvuma. 

Naibu Waziri Ajibu swali Lililomponza Kitwanga.....Asema Serikali Imekusudia Kujenga Nyumba 9500 Kwa Ajili Ya Askari Magereza

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusufu amejibu upya swali lililomponza bosi wake wa zamani, Charles Kitwanga.

Uamuzi wa kurudia swali hilo ulitolewa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisema swali hilo lilijibiwa katika hali ya ulevi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na wabunge wakaomba mwongozo kuhusu majibu yaliyotolewa.

Kitwanga aliondolewa katika nafasi yake na Rais John Magufuli baada ya kujibu ya swali hilo akiwa amelewa.

Leo, Masauni amejibu swali hilo namba 211 la Mbunge wa Viti Maalumu Devota Minja (Chadema) na kuonyesha utofauti mkubwa kati ya majibu yake na yale yaliyotolewa mwishoni mwa wiki na aliyekuwa Waziri wake.

Swali hilo ambalo awali lilikuwa namba 205, liliulizwa na Devota Minja akitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuboresha makazi ya polisi na askari magereza wanaoishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ukilinganisha na kazi zao kwa jamii.

Nyakati zote hizo, swali hilo limeulizwa na wabunge tofauti wa Chadema kutokana na Minja kutokuwapo, mara ya kwanza likiulizwa na Suzan Kiwanga (Mlimba) na leo Joseph Selasini wa Jimbo la Rombo.

Tofauti ya majibu ya Kitwanga, Masauni ametoa takwimu katika ujenzi wa nyumba 9,500 za Magereza nchi nzima ambapo amesema  tayari serikali imekwisha ingia mkataba na
Kampuni ya Poly Technologies ya China kujenga nyumba hizo.
 
Mhe. Masauni alibainisha kuwa  kupitia mkataba huo Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto iliyopo ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya askari wa jeshi hilo ambapo mahitaji kwa sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni nyumba 4,221 hivyo kupelekea upungufu wa nyumba 10,279.

“Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi, hivyo katika kukabiliana na tatizo hili Serikali imeendelea kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba na pia kujenga nyumba mpya”. Alisema Masauni.

Mhe. Masauni alifafanua  kuwa mgawanyo wa ujenzi wa nyumba hizo mpya ni Makao Makuu ya Magereza nyumba 472, Arusha nyumba 377, Dar es Salaam nyumba 952, Dodoma 356, Kagera 364, Kigoma 272, Kilimanjaro 390, Lindi 233, Manyara 206, Mara 378, Mbeya 622, Iringa 336, Morogoro 669, Mtwara 215, Mwanza 398, Pwani 384, Rukwa 358, Ruvuma 320, Shinyanga 337, Singida 299, Tabora 408, Tanga 382, KMKGM Dar es Salaam 219, Chuo cha Ukonga 115, Chuo cha Kiwira 183, Chuo cha Ruanda 62, Chuo KPF 27, Bohari Kuu 82 na Bwawani nyumba 84.

Aidha, Mhe. Masauni aliongeza kuwa kwa upande wa Jeshi la Polisi, Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar zitakazosaidia kupunguza tatizo la makazi kwa askari wa jeshi hilo.

Mhe. Masauni alilieleza bunge kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakavyokuwa inaimarika.

CCM: Hatutamuadhibu Kitwanga Mara Mbili

CCM imesema kitendo cha Rais John Magufuli kumvua uwaziri Charles Kitwanga kutokana na kuingia bungeni akiwa amelewa, kimedhihirisha kuwa bado kuna baadhi ya watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma, lakini hakitachukua hatua kwa kuwa ameshaadhibiwa.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka jana  alisema kitendo cha Kitwanga kuingia bungeni akiwa amelewa kimewapa fundisho na sasa wanajua kuwa kuna baadhi ya watumishi waliopewa dhamana na chama hicho, lakini wanakiuka miiko ya maadili ya utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume na taratibu zao.

Sendeka alisema licha ya kwamba Rais Magufuli amechukua hatua juu ya hilo na kutoa adhabu, CCM itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya wanasiasa waliopewa dhamana na chama hicho.

“Hatutasita kuchukua hatua endapo tutabaini kuna kada anayekiuka maadili ya viongozi wa umma,” alisema Sendeka.

Alisema CCM inampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi aliochukua dhidi ya Kitwanga kwa kuwa hatua hiyo imedhihirisha kauli aliyowahi kusema kwamba hataangalia mtu usoni wala kujali kabila au dini, ikiwa mtu huyo atakiuka miiko ya uongozi.

Kuhusu CCM kumuadhibu Kitwanga, Sendeka alisema adhabu aliyopewa na Rais inatosha. “Hukumu haitolewi mara mbili,” alisema Sendeka.

Kitwanga ambaye anatajwa kwenye sakata la utekelezaji mbovu wa mkataba wa kufunga vifaa vya kuchukua alama za vidole baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises, alivuliwa ukuu wa wizara hiyo nyeti baada ya kutinga ndani ya ukumbi wa Bunge Ijumaa asubuhi na kujibu maswali akiwa amelewa.

Hadi jana jioni, Rais Magufuli alikuwa bado hajajaza nafasi hiyo nyeti huku wananchi wakibashiri jina la mrithi wa Kitwanga kwa kuangalia jinsi marais waliopita walivyokuwa wakijaza nafasi kama wa kumpandisha naibu waziri wa wizara hiyo au nyingine, kumteua mtu anayemfahamu, kubadilisha mawaziri na kumrejesha aliyewahi kuwa waziri ama kuteua kutoka kwenye kanda anayotoka aliyetimuliwa.

Mara nyingi katika uteuzi wa mawaziri, viongozi wakuu wa nchi wamekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya manaibu kuwa mawaziri, kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka katika mkoa ambao anatokea waziri aliyeondolewa.

Mara zote saba ambazo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri alifuata utaratibu huo.

Alipomuondoa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye ni mbunge kutoka mkoa Kagera alimteua mbunge mwingine kutoka mkoa huo, Charles Mwijage kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.Kwa sasa Mwijage ni Waziri wa Viwanda na Biashara. 
Utaratibu huo unaweza kunufaisha wabunge sita wa majimbo yaliyopo mkoa wa Mwanza ambao ni Chalres Tizeba (Buchosa), Mansoor Hirani (Kwimba), Kiswaga Boniventura (Magu), Stanslaus Mabula (Nyamagana), William Ngeleja (Sengerema) na Richard Ndassa (Sumve).

Mbali na Kitwanga ambaye aliteuliwa kuwa waziri kutoka mkoa huo, Rais pia alimteua mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Iwapo Rais atatumia utaratibu wa kupandisha naibu waziri kuwa waziri, neema huenda ikamuangukia mbunge wa Kikwajuni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandishi Hamad Masauni au naibu mawaziri kutoka wizara nyingine. Katiba pia inampa Rais fursa ya kuteua wabunge 10 na tayari ameshatumia nafasi sita.

Familia Yasema Kifo cha Wilson Kabwe Hakikutokana na Mshtuko wa Kufukuzwa Kazi na Rais Magufuli


Familia ya Wilson Kabwe, aliyekuwa mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, imesema ndugu yao alishawatoa wasiwasi kuhusu tuhuma zilizosababisha kusimamishwa kazi na Rais John Magufuli na kwamba alitamani uchunguzi ufanyike haraka ili ukweli ujulikane. 
Kabwe aliyefariki dunia Mei 20 kwa ugonjwa wa saratani ya tezi dume jijini Dar es Salaam, alisimamishwa kazi na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni Aprili 19. 
Miongoni mwa makosa yaliyosababisha kusimamishwa kwake ni madai ya kusaini mkataba kwa kutumia sheria ndogo ya mwaka 2004 kutoza magari yanayotoka kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo (UBT) Sh4000 na mwingine wa Sh8,000 chini ya sheria ndogo mwaka 2009. 
Kulikuwa pia na madai ya kukithiri kwa rushwa katika kituo hicho hasa katika kutoa magari na ukodishwaji wa vyumba vya kupangisha, kinyume na utaratibu na kuongeza muda wa mzabuni aliyeingia mkataba na jiji wa maegesho ya magari. 
Akizungumza jana nyumbani kwao, Masaki jijini Dar es Salaam, mtoto wa marehemu, Joseph Kabwe alisema kifo cha baba yao hakikutokana na mshtuko wa kusimamishwa kazi, bali alianza kuugua muda mrefu na alishawaambia kuwa hana wasiwasi na tuhuma hizo, bali anataka uchunguzi ufanyike haraka. 
“Alikuwa na saratani ya tezi dume na alikuwa akitumia dawa za chemotherapy ambazo ni kali sana na zilisababisha kuathirika kwa ini. Hata siku baba anatumbuliwa pale darajani alisema hana wasiwasi kwa sababu kila kitu kiko sawa sawa,” alisema Joseph. 
“Baba alitutaka tusiwe na wasiwasi, tena mwenyewe alikuwa akisisitiza kuwa anatamani matokeo ya uchunguzi yatoke mapema ili ukweli ujulikane,” alisema. 
Jana msibani kulikuwa na viongozi tofauti wa ngazi ya mkoa waliofika kutoa pole. Kaimu mkurugenzi wa jiji aliyekuwapo msibani hapo, Sarah Yohana alisema Halmashauri ya Jiji inashiriki msiba huo kwa kuwa Kabwe alikuwa mtumishi wao. 
“Yule alikuwa mtumishi wa halmahsauri na ana haki zake kama mtumishi mwingine yoyote. Tutatoa jeneza, gari la kusafirishia maiti, chakula na rambirambi,” alisema Sarah. 
Sarah alisema alikabidhiwa ofisi na Kabwe tangu Novemba mwaka jana baada ya kwenda kutibiwa nchini India. Kuhusu taratibu za utumishi, alisema licha ya Rais kumsimamisha kazi, hawakuwahi kuona barua yoyote iliyoletwa inayohusu kusimamishwa kwake. 
“Inawezekana alipewa kwa njia nyingine, lakini sisi hatukuona barua ya kusimamishwa. Yule ni ‘presidential appointee’ (mteule wa Rais), yeye ndiye mwenye mamlaka na watu wake wa kufanya uchunguzi. Sisi hatujui, inawezekana wanafanya uchunguzi wao huko wenyewe,” alisema Sarah. 
Jana Msemaji wa familia hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Eliab Mkenga Kabwe alisema hawana ugomvi wowote na Serikali huku akimkana mtu aliyejitambulisha kuwa msemaji wa familia hiyo, Dk. Zawadi Machuve aliyetoa maelezo kwa waandishi wa habari juzi kuwa hawataki viongozi wa Serikali wakanyage msibani. 
Aliongeza kuwa familia hiyo inatambua na kuthamini mchango wa Serikali katika kugharamia matibabu na huduma zote za mazishi. 
Alisema Makonda aliyetoa tuhuma za Kabwe kabla ya Rais Magufuli kutangaza kumsimamisha kazi, anatarajiwa kufika msibani hapo muda wowote. 
“Mkuu wa Mkoa, Makonda bado hajafika hapa, lakini anaweza kufika wakati wowote. Unajua yeye ndiye mwenye mkoa wake kwa hiyo atafika tu wakati wowote,” alisema.
Mbali na viongozi wa jiji waliokuwapo kwenye msiba huo, viongozi wa mikoa mingine akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo na mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga walikuwapo msibani hapo. 
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, ambaye alikuwapo eneo hilo, ameshauri msiba huo uhamishiwe katika ukumbi wa Karimjee ikiwa ni kumpa heshima Kabwe aliyekuwa kiongozi wa jiji, lakini hakuna dalili za kufanya hivyo.

Saturday, May 21, 2016

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam , Willson Kabwe Afariki Dunia sababu hii hapa

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe ambaye April 19 mwaka huu alisimamishwa kazi na Rais Magufuli kwenye daraja la Nyerere amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na  Meya wa Jiji la Dar  es Salaam, Isaya Mwita
Kabwe amefikwa na mauti  akiwa nchini India kwa matibabu. Mungu ailaze mahala pema peponi roho ya marehemu. Amina
 

chips hatari kwa wajawazito



.
Hii ni kauli ya mtaalamu wa lishe wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Denis Mbinga katika mahojiano na Gazeti la Mtanzania.
Katika mahojiano hayo Mbinga amesema matatizo ya watoto kuzaliwa na vichwa vikubwa , mgongo wazi na magonjwa mengineyo katika siku za karibuni yameongezeka kutokana na ulaji wa vyakula visivyofaa na hasa chipsi na vile vilivyosindikwa viwandani.

Friday, May 20, 2016

Breaking News: Rais Magufuli Atengua Uteuzi wa Waziri Wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga Baada Ya Kuingia Bungeni Akiwa Amelewa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Charles Kitwanga kuanzia leo tarehe 20 Mei, 2016.

Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kufuatia kitendo cha Mheshimiwa Charles Kitwanga kuingia bungeni na kujibu swali linaloihusu wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwa amelewa.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

20 Mei, 2016