Monday, June 6, 2016

Taarifa ya Ofisi ya Spika kuthibitisha kupokea hoja ya kumeondoa madarakani Naibu Spika


Ofisi ya Spika imepokea taarifa ya kusudio la kuleta Bungeni Hoja ya kumwondoa madarakani Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb) iliyowasilishwa na Mbunge wa Simanjiro Mhe. Mhe. James Kinyasi Millya siku ya Jumatano tarehe 1 Juni, 2016.
 
Utaratibu huo ni wa Kikatiba na upo chini ya Ibara ya 85(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ambapo pia umeainishwa katika Kanuni ya 138 (1), ya kanuni za Kudumu za Bunge kuhusu utaratibu wa Kumwondoa Naibu Spika Madarakani.
 
Baada ya kupokea kusudio hilo, Kanuni za Bunge zinamtaka Spika kuiwasilisha hoja hiyo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ifanyiwe kazi.
 
Kutokana na msingi huo wa kikanuni, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai (Mb) anakusudia kuliwasilisha swala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kama Kanuni inavyoelekeza ambapo kamati hiyo itaangalia msingi wa hoja na endapo itaridhika, kanuni inaitaka Kamati kuwasilisha hoja hiyo Bungeni ili ijadiliwe. 
Aidha, Kanuni ya 138 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inamtaka Spika kukalia kiti wakati wa mjadala wa hoja ya kumwondoa Naibu Spika Madarakani.
 
Hivyo basi, suala lililowasilishwa na Mhe. James Kinyasi Millya kuhusu kusudio la kumwondoa Naibu Spika Madarakani, tayari limepokelewa na lipo katika Ofisi ya Spika kwa ajili ya utekelezaji wa masharti ya Kanuni.

Imetolewa na,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA
6 Juni, 2016.

Polisi Jijini Mwanza Wapambana na Majambazi kwa Saa 16.....Wakamata Silaha Nzito, Watatu Wauawa



Watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi,wameuawa katika majibizano ya risasi na askari polisi mkoani Mwanza,alfajiri ya kuamkia jana jumapili katika mapango ya mlima wa Utemini yaliyopo kata ya Mkolani jijini Mwanza.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza Ahmed Msangi,amewataja majambazi waliouwa katika majibizano ya risasi usiku kucha kuwa ni Omar Francis Kitaleti mkazi wa Nyegezi Kona,said Khamis Mbuli maarufu kama fundi bomba mkazi wa bugarika na jambazi mwingine ambaye jina lake bado halijafahamika.

Amesema majambazi hayo yalikuwa yamejificha kwenye mapango ya mlima wa Utemini kabla ya askari polisi kufanikiwa kuyaua.

Jambazi mmoja aliyeuawa ambaye hajafahamika jina lake mwenye umri kati ya miaka 20 hadi 25 alikuwa akiwashambulia polisi kwa kutumia bastola ambapo baada ya polisi kumpiga risasi walimpekua na kumkuta akiwa na bastola aina ya Chinese,iliyokuwa na risasi tatu ndani ya magazine,huku majambazi wengine waliokuwepo kwenye mapango hayo wakiendelea kujibishana kwa risasi na askari polisi.

Kamanda Msangi ameongeza kwamba Ijumaa Juni 3,askari polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama,walimkamata Omar Francis Kitaleti kwa jina maarufu kiberiti,mkazi wa Nyegezi Kijiweni ambaye alikuwa akituhumiwa kuhusika katika matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha kwenye maduka ya M-pesa,Tigo Pesa na Airtel money jijini Mwanza ambaye baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika katika matukio hayo na aliwataja wenzake anaoshirikiana nao na mahali walipojificha.

Amesema ilipotimu majira ya saa kumi na moja kamili jioni siku ya Jumamosi Juni 4,polisi walifika katika mlima huo na walipoyakaribia mapango hayo ghafla walianza kushambuliwa kwa risasi na majambazi waliokuwa wamejificha ndani ya mapango hayo.
Omary Francis Kitaleti @Kiberiti, mmoja wa majambazi aliyeuawa na wenzake kwa risasi.

Katika mapambano hayo ya risasi na askari polisi,risasi hizo ziliweza kumpata jambazi mwenzao aitwaye Omary Francis Kitaleti aliyekuwa anawaongoza askari polisi na kufariki dunia papo hapo, na risasi nyingine ilimjeruhi askari kwenye unyayo wa mguu wake wa kulia.

Amesema polisi kwa kutumia mbinu za medani za kivita waliweza kuzingira maeneo hayo ya mlima wa utemini hadi alfajiri ya kuamkia Jumapili Juni 5,huku wakijibishana risasi na majambazi hao na baada ya kuona yamezidiwa nguvu huku kukikaribia kupambazuka ndipo yalipoamua kuondoka ndani ya mapango hayo kwa kurusha bomu moja la kutupa kwa mkono huku yakizidisha mapigo ya risasi kwa kutumia silaha walizokuwa nazo.

Ameongeza kuwa polisi wamekamata bunduki moja aina ya SMG iliyokuwa na risasi nane na kisu kimoja.

Kamanda Msangi amesema majambazi watatu walifanikiwa kutoroka kutoka kwenye mapango hayo kuelekea maeneo ya Nyasaka na baada ya jambazi mmoja kubaini kuwa askari polisi walikua wanamfuatilia alitoa bunduki  na kutaka kuwapiga askari polisi lakini polisi waliweza kumuwahi na kumfyatulia risasi sehemu mbalimbali za mwili wake na kufariki dunia papo hapo.

Amesema askari polisi wamefanya upekuzi kwenye mapango ya mlima wa Utemini na kufanikiwa kupata vitu mbalimbali vilivyoachwa na majambazi hao ambavyo ni pamoja na risasi nne,kisu kimoja chenye damu,kofia ya kuficha uso nyeusi moja (mask),jiko la stove,masufuria ya kupikia, unga wa mahindi,sukari,dagaa,chakula kilichopikwa,ngoma mbalimbali,na simu tatu za mkononi.

Askari aliyejeruhiwa amelazwa hospitali ya rufaa ya bugando na hali yake inaendelea vizuri,polisi bado wanaendelea na msako wa kuwatafuta majambazi waliofanikiwa kutoroka.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo alitembelea kwenye mapango ya Utemini na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi katika kuwafichua wahalifu

Thursday, June 2, 2016

MASAUNI AONGOZA VIONGOZI WA SERIKALI KUHANI MSIBA WA WALIOCHINJWA KITONGOJI CHA KIBATINI MKOANI TANGA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia) akimpa pole Hussein Mkola ambaye ni mtoto wa marehemu Mkola Hussein ambaye alichinjwa na watu wanaohofiwa kuwa majambazi mwanzoni mwa wiki hii katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, mkoani Tanga. Masauni alifanya ziara katika msitu wa Mapangopori ya Amboni linalodaiwa kuwa ni njia kuu ya wauaji hao, na baadaye alienda kutoa pole katika familia nane zilizofiwa katika kitongoji hicho.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati) akimsikiliza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo wakati alipokuwa anawasili msibani katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, mkoani Tanga, ambapo watu wanane walichinjwa na watu wanaohofiwa kuwa majambazi. Masauni alifanya ziara katika msitu wa Mapangopori ya Amboni linalodaiwa kuwa ni njia kuu ya wauaji hao, na baadaye alienda kutoa pole katika familia hizo zilizofiwa katika kitongoji hicho. Kushoto ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiwapa pole wanafamilia ya marehemu Mkola Hussein ambaye alichinjwa na watu wanaohofiwa kuwa majambazi mwanzoni mwa wiki hii katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, mkoani Tanga. Masauni alifanya ziara katika msitu wa Mapangopori ya Amboni linalodaiwa kuwa ni njia kuu ya wauaji hao, na baadaye alienda kutoa pole katika familia nane zilizofiwa katika kitongoji hicho. Nyuma ya Naibu Waziri ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo akiwaonyesha Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange (wapili kushoto) na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu (watatu kushoto), nyumba ya kwanza katika Kitongoji cha Kibatini walioivamia watu wanaohofiwa kuwa majambazi na kufanya mauaji. Naibu Waziri na Viongozi hao walienda kutoa pole katika familia zilizofiwa katika Kitongoji hicho kilichopo katika Kata ya Mzizima, mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akitoa salamu za pole kwa ndugu wa marehemu Mkola Hussein pamoja na wananchi wa Kitongoji cha Kibatini kulipotokea mauaji kwa watu wanane ambao walichinjwa na watu wanaohofiwa kuwa majambazi mwanzoni mwa wiki hii katika Kitongoji hicho kilichopo Kata ya Mzizima, mkoani Tanga. Katika hotuba yake Masauni alisema Serikali imesikitishwa na tukio hilo na itahakikisha inawakamata wauaji wote waliofanya ukatili huo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia) wakijadiliana jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange kabla ya kwenda kutoa pole kwa familia ya wafiwa katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, mkoani Tanga ambapo watu wanane walichinjwa na watu wanaohofiwa kuwa majambazi. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wednesday, June 1, 2016

Afikishwa Mahakamani kwa Tuhuma za Kumuua Mkewe Baada ya Kumkuta Akifanya Mapenzi na Mwanaume Mwingine

Mkazi wa Kijiji cha Ussonge, Kata ya Nyandekwa, Mkungu Kodoli (50) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora akikabiliwa na mashtaka ya kumuua mkewe.

Akimsomea mashtaka jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Ajali Milanzi, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Frank Matiku alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 26, mwaka huu saa 4.30 usiku nyumbani kwake.

Matiku alidai kuwa mshtakiwa alimpiga mkewe, Nsungurwa Dotto (46) kwa fimbo kichwani na kusababisha kifo chake.

Alidai chanzo cha mauaji hayo ni baada ya mshtakiwa kumfumania mkewe akifanya mapenzi na mwanaume mwingine.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu kitu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi za mauaji hadi atapofikishwa Mahakama Kuu baada ya upelelezi kukamilika.

Matiku alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na Hakimu Milanzi kuiahirisha hadi Juni 14, itakapotajwa tena.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya June 2

Wapinzani Wawasilisha Hoja ya Kumwondoa Madarakani Naibu Spika, Dr Tulia Ackson

Wabunge wa upinzani wamewasilisha kwa Spika wa Bunge hoja ya kumwondoa madarakani Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa kutokuwa na imani naye.

Hatua hiyo imefikiwa na wabunge hao kufuatia kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi wa Dk Tulia anapokalia kiti cha Spika.

Tangu Jumanne wiki hii, wabunge hao wamekuwa wakisusa vikao vinavyoongozwa na kiongozi huyo kwa madai anaminya demokrasia.

Walifikia uamuzi huo baada ya Dk Tulia kuzuia kujadiliwa hoja ya kufukuzwa kwa wanafunzi zaidi ya 7,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) iliyowasilishwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na kukatisha mjadala wa bajeti ya maji.

Kitendo hicho kiliwafanya wabunge wote wa upinzani kupingana na maamuzi ya Dk Tulia, jambo lililosababisha watolewe bungeni.

Kutokana na hali hiyo wabunge hao kupitia Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya akisindikizwa na Mbunge wa Kibamba, John Myika wa Chadema na Mbunge wa Konde wa CUF, Khatibu Said Haji waliwasilisha hoja hiyo kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah baada ya Spika, Job Ndugai kutokuwapo bungeni.

Hoja hiyo iliwasilishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 138 (1) ambayo inaeleza utaratibu wa jinsi ya kumwondoa Naibu Spika.

Kanuni hiyo inasema, “Utaratibu wa kumwondoa Naibu Spika madarakani chini ya Ibara ya 85(4)(c) ya Katiba utakuwa kama ule wa kumwondoa Spika, isipokuwa tu taarifa ya kusudio la kumwondoa Naibu Spika madarakani inayoeleza sababu kamili za kuleta hoja hiyo, itapelekwa kwa Spika ambaye ataiwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuijadili.”

Fasili ya pili ya Kanuni hiyo inasema: “Endapo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itaridhika kuwa zipo tuhuma mahususi dhidi ya Naibu Spika zinazohusu uvunjaji wa Katiba, Sheria au Kanuni zinazoongoza Shughuli za Bunge, basi Kamati hiyo itaidhinisha kuwa hoja hiyo ipelekwe bungeni ili iamuliwe.”

Kwa mujibu wa Ibara ya 85(4)(c), Naibu Spika atakoma kuwa Naibu Spika na ataacha kiti cha Naibu Spika endapo ataondolewa kwenye madaraka ya Naibu Spika kwa azimio la Bunge.

Akizungumzia uwasilishwaji wa hoja hiyo, Millya alisema taarifa zaidi watatoa leo kuhusu msimamo wao huo.

Dk Tulia aliwataka wabunge wenye malalamiko juu ya utaratibu wa uendeshaji wa shughuli za Bunge kukata rufaa kwa kufuata Kanuni za Bunge.

Alisema kanuni ndogo ya 5(2) inasema Spika atawajibika kutilia nguvu kanuni zote za Bunge na 5(3) inasema Spika anaweza kumtaka mbunge yeyote anayekiuka kanuni hizi kujirekebisha mara moja.

Alisema kwa hiyo mbunge yoyote asiyeridhika, kanuni za Bunge zinamruhusu kukata rufaa na zinamweleza nini cha kufanya.

Mauaji ya Kutisha: Watu 8 Wakamatwa Kwa Mwenyekiti wa Kitongoji na Kuchinjwa Kinyama

MAUAJI ya Watanzania kwa njia ya kuchinjwa yanaendelea kushika kasi baada ya usiku wa kuamkia jana wakazi wanane wa kitongoji cha Kibatini, kata ya Mzizima jijini Tanga kukusanywa kwa mwenyekiti wa kitongoji na kisha kuuawa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana.

Watu hao ambao inadaiwa kuwa ni majambazi walivamia usiku wa kuamkia jana kwa kuvunja milango ya nyumba tatu ambazo wakazi hao walikuwa wamelala na kuwachinja kisha kuiba biskuti, mchele na sukari na kutokomea navyo kusikojulikana.

Wauaji hao inadaiwa wana uhusiano na wahalifu ambao wamekuwa wakijificha ndani ya mapango ya Majimoto na kujihusisha na matukio kadhaa ya uvamizi ili kupora vyakula na kusababisha mauaji ya wakazi wa Jiji la Tanga, ikiwamo katika duka kuu la Central Bakery mwishoni mwa Aprili mwaka huu.

Mmoja wa shuhuda wa mauaji hayo, Kea Leonard (70) ambaye pia ni mkazi wa Kibatini, katika mahojiano jana alisema wanaamini kwamba chanzo cha mauaji ya wenzao ni kulipiza kisasi.

“Wiki iliyopita majira ya saa tano asubuhi hapa tulikamata vijana saba kati ya wanane wenye umri wa kama miaka 13 ambao walikuwa wakiranda randa hapa kitongojini ili kutafuta namna ya kuvuka mto kwenda ng’ambo ya pili na ndipo mmoja wao alipotutoroka,” alieleza Leonard na kuongeza:

“Watoto hao tulipowaweka chini ya ulinzi na kuwahoji tukaanza kuwatilia shaka hivyo mwenyekiti aliamua kuripoti Polisi na ndipo hao wakawachukua kwa ajili ya mahojiano na hatukufuatilia tena kujua kwamba waliachiwa au la kwa sababu hao watoto sio wenyeji wala wakazi wa eneo hili.”

Aliongeza kwamba wakati wahalifu hao wanavamia nyumba ya mjumbe wa serikali ya kitongoji kabla ya kumtoa nje walisikia mmoja wa watu hao akimhoji kuhusu mahali walipopelekwa watoto saba.

Diwani wa Kata ya Mzizima, Fredrick Charles alizungumza na waandishi wa habari na kuthibitisha kwamba kati ya watu waliokufa mmoja ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mleni uliopo kwenye kata hiyo.

“Hali ya usalama hapa kwetu Mzizima si shwari kwa sababu wananchi wangu wa Kibatini wamevamiwa na kuchinjwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa sita usiku,” alisema Chiluba. 
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mleni kilichopo kitongoji hicho, Shabani Amani alisema wamepatwa na hofu kubwa kuhusu matukio hayo.

“Tunadhani kuna mapungufu katika suala la ulinzi hapa kwa sababu baada ya kutokea matukio kadhaa eneo letu hasa baada ya kudaiwa kwamba mapango waliyojificha wahalifu yako hapa jirani na kwetu kikosikazi cha mchanganyiko wa askari polisi na wa JWTZ wanafanya doria kwa saa 24 lakini tunashangaa kwa nini matukio yanaendelea,” alisema Amani.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul alithibitisha mauaji hayo. “Mei 30, mwaka huu majambazi waliokuwa na visu na mapanga walivamia kaya tatu na kuua wananchi majira ya saa saba usiku,” alisema Kamanda Paul.

Aliwataja waliouawa ni Issa Hussein (50) ambaye ni mmiliki wa kaya hiyo pamoja na kuibwa biskuti, mchele na sukari katika duka dogo. Wa kaya nyingine ni Mkola Hussein (40) na Hamis Issa (20), Hamis Issa (20) na aliyemtaja kwa jina la Mikidadi (70).

Kamanda aliwataja marehemu wengine ni Mahamud (35) ambaye ni mkwe wa Mikidadi, Issa Ramadhani (25), Kadir (25) na Salum ambao ni wachunga ng’ombe kijijini humo. 
Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mke wa marehemu Mkola aitwaye Aisha Saidi, alisema walipofika nyumbani hapo waligonga mlango na kumtoa nje Mkola na kuondoka naye.

“Nimeachwa mjane na watoto sita... Baada ya hao watu kuingia walimkamata Mkola na kumdai aeleze kwamba watoto wao saba wamepelekwa wapi na alipojibu sijui wakamtoa nje na kumkusanya pamoja na wanakijiji hao wengine na kuwachinja eti tu kwa sababu hawakutaja mahali walipopelekwa watoto,” alisema Aisha.

Katika hatua nyingine, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa kupokea taarifa za vitendo vya mauaji ya kikatili vinavyoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini.

“Wimbi hili la matukio ya vitendo vya mauaji na ukatili uliojitokeza kwa kufuatana mwezi Mei 2016 yanavunja haki ya kuishi ambayo ndio msingi wa haki zote za binadamu kwa ujumla wake.

"Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali mauaji haya yote na matendo yote ya kikatili dhidi ya mwanadamu yanapotokea popote nchini,” ilieleza taarifa ya Mwenyekiti wa Tume, Bahame Nyanduga.

Tume iliishauri serikali kupitia Jeshi la Polisi ichukue hatua mahsusi kuhakikisha ulinzi wa wananchi dhidi ya mauaji na vitendo hivi, kwani jukumu la kwanza la kuhakikisha usalama wa wananchi ni jukumu la serikali. 
Jeshi la Polisi lihakikishe watu wote waliohusika kutekeleza mauaji haya wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake, ilieleza.